Wajumbe wa Mradi wa Pamoja wa Vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho (KCJE LTD) wamefanya ziara ya mafunzo katika Chama Kikuu cha Ushirika MILAMBO, wilayani Urambo, mkoa wa Tabora.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa kujifunza mbinu bora za uendeshaji wa vyama vya ushirika, hususan katika maeneo ya utawala, masuala ya kifedha, usimamizi wa miradi, na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa shughuli za chama.
Wakiwa MILAMBO, wajumbe walipata fursa ya kukutana na uongozi wa chama, ambapo walijadiliana kwa kina kuhusu namna chama hicho kinavyotekeleza shughuli zake, hasa katika eneo la uwekezaji na usimamizi wa miradi.
Kwa upande wake, uongozi wa MILAMBO CU LTD ulitoa ukaribisho wa kipekee, na kuelezea historia ya chama, mafanikio yaliyopatikana, pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo katika kukuza ushirika wa kisasa.
Ziara hii ni sehemu ya jitihada endelevu za kubadilishana uzoefu na kukuza ushirikiano kati ya vyama vya ushirika nchini, ili kuongeza ufanisi na tija katika sekta ya ushirika.




